WIZARA YA MAJI YASIMAMIA UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YA WAZIRI MKUU -KILIMANJARO
Serikali kupitia Wizara ya Maji imeanza kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt Mwigulu Nchemba, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Hatua hiyo imeanza katika Wilaya za Moshi, hususan Kata za Kimochi, Mabogini na Uru Mashariki ambako wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.
Akizungumza Februari 25, 2026 wakati wa kusikiliza kero za wananchi, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, ameeleza kuwa ndani ya miezi mitatu changamoto ya maji itakuwa imepatiwa ufumbuzi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa uhakika na endelevu kwa zaidi ya wananchi 16,000 wa eneo hilo.
Aidha, Mhe. Kundo ametembelea kata za Mabogini, Kimochi na Uru Mashariki kukagua hali ya upatikanaji wa maji na maendeleo ya miradi inayoendelea. Amesema utekelezaji huo unatokana na maelekezo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa wakati wa ziara yake mkoani Kilimanjaro, na kwamba kwa niaba ya Waziri wa Maji wizara imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo Machi 28, 2026 wananchi wa Kata ya Mabogini wanakuwa wameanza kupata huduma ya maji safi na salama.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kusimamia kwa karibu miradi ya maji ili wananchi wapate huduma bora na ya kuaminika.
Katika hatua nyingine, Wizara imeielekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kuongeza uzalishaji wa maji katika Kata ya Kimochi ili kukidhi mahitaji ya sasa na yanayoongezeka ya wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Mhe. Morisi Makoi, alisema bado kuna maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa maji na kupongeza jitihada za serikali. Amebainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha ya wananchi waliolazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
