Media Centre » News and Events

Kiongozi mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aipongeza Muwsa mradi wa maji Njiapanda

Moshi.Zaidi ya wananchi 13,734 wa kata ya njia panda na maeneo jirani, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wanatarajia kuondokana na adha ya maji safi na salama inayowakabili, baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Miwaleni-Njiapanda ambao utagharimu zaidi ya Sh 2.3bilion hadi kukamilika.

Mradi huo ambao unatekelezwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi (Muwsa) unatarajiwa kukamilika mwezi septemba mwaka huu na tayari serikali imeshatoa Sh 1bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma Mkurugenzi wa Muwsa, Kija Limbe amesema mradi huo utakapokamilika utaboresha hali ya huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya Miwaleni,Mabungo na Kata ya Njia Panda.

"Mradi huu utagarimu Sh 2.37bilioni hadi utakapokamilika na mpaka sasa utekelezaji umefikia asilimia 45 na unatarajiwa kukamilika mwezi septemba mwaka huu ambapo utawanufaisha zaidi ya wananchi 13,734"

Akizungumza Kiongozi wa Mbio wa mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Nyanzabara Geraruma baada ya kukagua mradi huo,amepongeza jitihada zinazofanywa na Muwsa na kuwataka kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

"Mradi huu ni mzuri niwapongeze watendaji na wataakamu waliopewa dhamana ya kuusimamia, niombe mzingatie suala la muda, ili uweze kukamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi".

Aidha kiongozi huyo amewataka wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) kuunda jumuiya za watumia maji na kuhakikisha wanazisimamia.

"Undeni jumuiya za watumia maji na mzifuatilie zinafanyaje kazi,kama wananchi wanapata huduma kwa ufasaha, miundombinu inasimamiwaje na kama kuna maboresho yanafanyika kwa wakati".

Baadhi ya wakazi wa kata ya Njia panda  na maeneo jirani, wamesema kukamilika kwa mradi huo,kutawawezesha kuondokana na adha ya maji, ambayo imewatesa kwa zaidi ya miaka 40.

"Tumekuwa na shida ya maji kwa muda mrefu katika eneo letu la njia panda kwa muda mrefu, na tunaamini kukamilika kwa mradi huu kutaondoa changamoto hiyo na kutuwezesha sasa kupata muda wa kufanya shughuli za kimaendeleo"amesema Anna Ngowi mkazi wa Njia panda.