Media Centre » News and Events

Mamlaka ya Maji Safi Mjini MOSHI yawa bora kwa kipindi cha Miaka Minne

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi,(MUWSA) Joyce Msiru akizungumza wakati wa utamburisho wa wajumbe wa Bodi ya Mamlaka hiyo kwa katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji,Prof Kitila Mkumbo alipotembelea Mamlaka hiyo.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mji wa Moshi (MUWSA), Joyce Msiru, ameiwezesha mamlaka hiyo kuwa bora kati ya mamlaka na jumuiya ya mamlaka za udhibiti wa maji na nishati Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Taarifa zaidi zimesema mtendaji huyo ambaye mkataba wake wa miaka minne na MUWSA umemalizika Oktoba 9, mwaka huu, amehamishiwa wilayani Same kuendelea na majukumu katika mamlaka ya maji eneo hilo.

Kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa MUWSA, Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo, chini ya Mwenyekiti Profesa Jaffari Kigeghesho, Septemba 9, mwaka huu, ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, ikiomba wizara imwongezee mkataba mwingine, ili aendelee kusimamia mamlaka hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, alikiri kupokea barua hiyo kutoka Bodi ya Wakurugenzi ya MUWSA.

“Ni kweli tuliipata barua yao, lakini ombi lao lilikataliwa, na atapangiwa majukumu mengine, pia tumeshateua mkurugenzi mwingine,” alisema Profesa Mkumbo.

Sehemu ya barua ya Bodi ya Wakurugenzi ya MUWSA kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji ilisema: “Bodi ya Wakurugenzi imeridhika na utendaji wa kazi wa Bibi Joyce Ally Msiru ambaye ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa kipindi cha miaka minne.

“Bibi Joyce Ally Msiru aliteuliwa kuongoza Mamlaka kwa kipindi cha miaka minne kuanzia tarehe 10 Oktoba 2015 hadi 09 Oktoba 2019 kwa barua yenye kumbukumbu namba CFA/242/547/01’B’/12 ya tarehe 13 Oktoba 2015.

“Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne alichoongoza Bibi Joyce Ally Msiru ni kudhibiti upotevu wa maji kutoka asilimia 23.2 iliyokuwepo mwezi Oktoba, 2015 alipoteuliwa hadi kufikia wastani wa asilimia 19.9 mwezi  Agosti, 2019.

“Kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na viunga vyake kwa wastani wa saa 23.5 kwa siku kwa sasa, ikilinganishwa na wastani wa saa 23 ya Oktoba 2015

“Kuongeza vyanzo saba vya maji ambavyo vimeongeza uwezo wa uzalishaji kwa mita za ujazo 14,862 kwa siku.

“Kuongeza mtandao wa usambazaji wa majisafi kwa kilometa 355.91 toka kilometa 371.35 Oktoba 2015 hadi kilomita 727.26 Agosti 2019.

“Kuongeza urefu wa mtandao wa majitaka kwa kilometa 8.66 kutoka kilomita 58.3 Oktoba 2015 hadi kilomita 66.96 Agosti 2019.

“Kuongeza wateja 12,823 wa majisafi kutoka wateja 24,481 Oktoba 2015 hadi kufikia wateja 37,304 mwezi Agosti 2019.

“Kuongeza wateja wapya 272 wa majitaka kutoka wateja 2,664 mwezi Oktoba 2015 hadi kufikia wateja 2,936 mwezi Agosti 2019, ufanisi wa makusanyo umefikia wastani wa asilimia 95 ukilinganisha na asilimia 89 mwezi Juni 2015.

“Utekelezaji wa miradi 9 ya kuboresha huduma ya majisafi na 2 ya kuboresha huduma ya majitaka ambayo imegharimu shilingi bilioni 5.9.

“Mamlaka imeshiriki katika kutekeleza miradi iliyoko nje ya eneo lake la huduma baada ya kupewa maelekezo na Wizara ya Maji. Miradi hiyo inagharimu Tsh bilioni 28.78.

“Upatikanaji wa hati safi za hesabu kwa kipindi chote cha miaka minne aliyoongoza Mamlaka.

“MUWSA kuwa mamlaka bora kwenye utoaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 na 2017/2018.

“Mamlaka kuwa mshindi wa mamlaka bora kati ya mamlaka na jumuiya ya mamlaka za udhibiti wa maji na nishati Afrika Mashariki Kati na Kusini kwa mwaka 2016/2017.”