Media Centre » News and Events

MBUNGE PROF PATRICK NDAKIDEMI ATEMBELEA NA KUKAGUA MRADI WA MAJI KATA YA MBOKOMU

MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro,  Prof. Patrick Ndakidemi amesema serikali ya awamu ya sita imejidhatiti kuhakikisha inamaliza kero ya maji inayowakabili wananchi. 

Prof. Ndakidemi alitoa kauli hiyo jana wakati alipoongozana na Diwani wa kata ya Mbokomu, Rafael Materu,  Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhan Mahanyu na Mkurugenzi wa MUWSA Eng. Kija Limbe kukagua Mradi wa maji Kata ya Mbokomu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi ya kata ya Mbokomu Mbunge huyo alisema kuwa,  serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha miradi mbalimbali inakamilika ikiwemo miradi ya maji.

"Niishukuru serikali inayoongozwa  na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za kutatua kero ya maji katika kata hii ya Mbokomu kwa kuleta mradi huu mkubwa" alisema Prof. Ndakidemi. 

Mbunge huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuhakikisha wanaitunza na kuilinda miradi inayoletwa na serikali ili iweze kudumu kwa muda mrefu. 

Awali akiwasilisha taarifa yake, Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mhandisi Kija Limbe alisema kuwa, mradi huo wenye thamani ya milioni 486 na unatekelezwa na MUWSA na unategewewa kutatua kero ya uhaba wa maji unaokabili wananchi wa Kata ya Mbokomu. 

Mkurugenzi huyo aliwaeleza wananchi kuwa taasisi hiyo iko Mbokomu kisheria kama taasisi nyingine zinazopangiwa kutekeleza majukumu ya kiserekali katika kuwahudumia wananchi, na akawaomba ushirikiano ìli MUWSA iwape huduma.

Akiongea na wananchi katika mkutano huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi vijijini Ramadhan Mahanyu aliwapongeza mbunge na diwani kwa jitihada za kuitetea kata ya Mbokomu na kuleta miradi ya maendeleo.

Katibu huyo alikemea  vikali wale wanaobeza shughuli za kiutendaji zinazofanywa na MUWSA na kuwafahamisha kuwa hakuna tofauti ya kiutendaji kati ya MUWSA na RUWASA kwani wote wanatekeleza jukumu moja la kuwapatia wananchi huduma ya maji na wanawajibika katika wizara moja.

Amewataka wananchi wa Mbokomu kutunza miundombinu inayojengwa na vyanzo vya maji huko msituni ili upatikanaji wa huduma ya maji uwe endelevu.

Akitoa neno la shukrani, diwani wa kata hiyo Mhe Rafael Materu aliwashukuru watendaji wote wa MUWSA kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwapatia wananchi maji.