Mbunge wa JIMBO La Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi akiongozana na diwani wa Kata ya Mabogini Dr. Bibiana Massawe, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhan Mahanyu na Mkugenzi wa MUWSA Eng. Kija Limbe walitembelea na kukagua Mradi wa maji Kata ya Mabogini unaolenga kuhudumia vijiji vya Maendeleo, Mtakuja na Mserekia.
Akitoa taarifa, Eng. Kija Limbe alieleza kuwa mradi huo una thamani ya Tsh milioni 500 na unatekelezwa na MUWSA kwa fedha zilizotolewa na Rais Samia kupitia Mkopo wa UVIKO 19.
Mbali na mradi wa maji, mbunge aliwaeleza wananchi kuwa miradi mbalimbali imeshatekelezwa katika kata ya Mabogini ikiwepo ya ujenzi wa Madarasa 15 ya UVIKO 19 katika sekondari za Mpirani (8) na Mabogini (7) ambazo zimegharimu shilingi milioni 300. Mradi mwingine mkubwa unaotekelezwa Mabogini ni ule wa ujenzi wa barabara ya Gate Fonga hadi Kahe kwa kiwango cha changarawe wenye thamani ya Sh 358 milioni.
Akiongea na wananchi katika mkutano huo wa hadhara, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi vijijini Ramadhan Mahanyu alimshukuru mbunge na diwani kwa jitihada za kuitetea kata ya Mabogini na kuleta miradi ya maendeleo. Aliwashauri wananchi waendelee kuiunga mkono serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani kazi zilizofanyika kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja zinaonekana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mabogini Athuman Kitia na mwenezi wa kata Ndugu Hassan Kajembe kwa niaba ya wananchi waliishukuru Serikali na hususani Mama Samia, Mbunge, Diwani na watendaji mbalimbali wa serikali kwa miradi inayoelekezwa na kutekelezwa katika kata ya Mabogini.