Media Centre » News and Events

Moshi Watenga Sh50mil. Kupanua Huduma ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka mjini Moshi (MUWSA), imetenga Sh51 milioni kuweka kilomita 18.70 za mtandao wa maji safi katika maeneo mbalimbali ya mji huo.Katika taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo, Amina Mbarouk ilisema maeneo yatakayopata huduma hiyo ni Moshi Technical, Shiri Mgungani, Msaranga, Mabogini, Mjohoroni, Shiri Matunda na maeneo ya chini ya Msafiri Lenguyama.

Alisema hivi sasa mamlaka hiyo inatoa huduma ya majisafi kwa asilimia 98 kwa manispaa na asilimia 44 ya wakazi wanapata huduma ya majitaka.Mbarouk alisema yapo maeneo ambayo hayapati maji kwa saa 24, kama vile Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) na Shanty Town.

Mbarouk alisema kutokana na tatizo hilo,  mamlaka hiyo inashirikiana na Wizara ya Maji kupitia mradi wa program ya maendeleo ya katika sekta ya maji (WSDP) kutafuta vyanzo vya maji vya uhakika.Alisema kupitia WSDP na mamlaka hiyo wataingeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 24,500 hadi mita za ujazo 45,000 ifikapo mwaka 2015 na mita za ujazo 67,000 itapofika mwaka 2025.

Mbarouk alisema chanzo cha chemchem ni kipo katika eneo la Kikafu na kwamba mamlaka hiyo, itachimba visima vitano virefu katika maeneo ya KCMC, Rau na chuo cha Mwenge.Alisema pia kupitia mradi huo MUWSA imepanga kukarabati na kujenga matenki mapya ya kuhifadhia maji ili kukidhi mahitaji ya watumiaji.

Makamu mwenyekiti huyo alisema vilevile MUWSA imetenga Sh74 milioni kwa ajili ya ujenzi wa wa kilometa 2.8 za mtandao wa majitaka katika maeneo ya Long’ui B, Rau, Majengo na Pasua.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Antony Kasonta alisema mamlaka hiyo inakabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwamo upotevu wa maji kwa asilimia 27, kuwa na wateja wachache wa majitaka katika maeneo ambayo mtandao unapita.

Alisema matatizo mengine ni matumizi yasiyo sahihi ya mtandao wa majitaka kama kuweka matambara, mifuko ya plastiki na vitu vigumu ambavyo vinasababisha mtandao kuziba.

Source: Rehema Matowo, Moshi.