Media Centre » News and Events

MUWSA na mkakati wa kuongeza uzalishaji majisafi

MAMLAKA ya Majisafi na Utunzaji wa Mazingira Moshi (MUWSA) ni moja ya mamlaka zilizoanzishwa mwaka 1998 ikiwa na lengo la kuwapatia wananchi huduma ya majisafi na salama.

Kabla ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo katika miaka ya 1960 wananchi wa mji wa Moshi walikuwa wakipata maji kutoka chemchem za Nsere na Shiri kwa kutumia bomba moja kubwa lililofanyiwa matoleo ya usambazaji.

Mwaka 1974 hadi 1994, uliandaliwa mpango wa mji wa Moshi lengo likiwa ni kuimarisha miundombinu ikiwamo mfumo wa usambazaji majisafi.

Pamoja na mambo mengine mpango huo ulizingatia umuhimu wa kuondoa tatizo la matumizi mabaya ya majisafi yaliyopatikana na kuhakikisha maji yanayopatikana yanaleta tija katika maendeleo ya mji wa Moshi.

Katika kuhakikisha wananchi wa mji huo wanapata huduma ya maji safi na salama, serikali na washirika wake wa maendeleo waliamua kuwekeza kwenye sekta ya maji katika mji wa Moshi.

Mmoja wa washirika hao wa maendeleo wa serikali ya Tanzania ni serikali ya Ujerumani kupitia mashirika yake ya maendeleo kama GTZ na KfW yaliyofadhili mradi wa ukarabati wa mtandao wa usambazaji wa maji ulioanza mwaka 1999 hadi mwaka 2003.

Lengo la mradi huo ni kuongeza kiasi cha majisafi yanayozalishwa kutoka kwenye vyanzo hadi kwenye matanki pamoja na upanuzi wa mtandao wa usambazaji majisafi.

Moja ya kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa bomba mbili kubwa zenye urefu wa kilometa 16 zenye kipenyo cha kati ya mita 300 na mita 400.

Anthony Kasonta ni Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya MUWSA ambaye licha ya kuelezea changamoto zinazoikabili mamlaka yake, anaweka wazi mafanikio katika utoaji huduma ya majisafi kwa wakazi wa Moshi.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, MUWSA imekuwa na mafanikio makubwa ikiwamo utunzaji mazingira maeneo ya vyanzo vyote vikuu vya Nsere na Shiri kulingana na sheria ya maji nchini na kupata cheti cha utunzaji bora wa mazingira kutoka Bonde la Mto Pangani.

Mkurugenzi huyo anataja mafanikio mengine kuwa ni kuongeza kilometa za mraba 41.224 za mtandao wa majisafi na kilometa za mraba 5.787 za mtandao wa majitaka.

Aidha anasema mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti upotevu wa maji kutoka wastani wa asilimia 29 mwaka 2007/2008 hadi kufikia aslimia 27 za sasa lengo likiwa ni kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2013/2014.

Kwa upande wa mapato, Kasonta anasema ukusanyaji wake umeongezeka kutoka sh bilioni 2.281 mwaka 2006/2007 hadi kufikia sh bilioni 2.577 mwaka 2009/2010.

Pamoja na mafanikio hayo, MUWSA inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo kiwango kidogo cha majisafi kinachochangiwa na ukuaji wa mji wa Moshi hivyo kuongezeka kwa mahitaji huku kukiwa na idadi ndogo ya wateja wenye viwanda wanaotumia maji ya mamlaka hiyo.

Ni miaka kumi sasa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mahitaji ya maji kwa mji wa Moshi yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku ikilinganishwa na uzalishaji.

Mkurugenzi huyo anasema kuwa kwa sasa uzalishaji majisafi kwa siku ni mita za ujazo 25,500 ikilinganishwa na mahitaji ya mita za ujazo 38,485 kwa siku.

Anasema kutokana na tafiti mbalimbali na ukuaji wa mji huu, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2015 mahitaji ya majisafi yatafikia mita za ujazo 45,000 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 80 la uwezo wa uzalishaji katika vyanzo vilivyopo sasa.

Anafafanua kuwa kupitia mradi wa programu ya maendeleo ya sekta ya maji na mpango mkakati wa 2010/2015; MUWSA imejipanga kuongeza uzalishaji wa majisafi kutoka mita za ujazo 25,500 za sasa hadi kufikia mita za ujazo 45,000 ifikapo mwaka 2015 na mita za ujazo 67,000 ifikapo mwaka 2025.

Kila binadamu hujiwekea mipango ya muda mfupi na ya muda mrefu vivyo hivyo MUWSA nayo ina mipango ya muda mrefu ya miaka 50 ijayo katika kuhakikisha inatoa huduma bora zaidi ya majisafi na majitaka.

Chini ya mipango hiyo, mamlaka imepanga kuwa na vyanzo vipya vya majisafi ikiwamo chemchemi ya Miwaleni itakayozalisha mita za ujazo 25,000 lengo ni kukidhi mahitaji ya watu.

Mpango mwingine ni kupata eneo jipya na teknolojia mpya ya usafishaji wa majitaka ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa mji wa Moshi na kuendelea kuboresha mazingira.

Source: Charles Ndagulla