Mradi huo ambao umegharimu Sh2.378 bilioni hadi kukamilika, umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) kwa fedha kutoka serikalini na utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100 na zaidi ya wananchi 13,734, wamefikiwa na huduma.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 16, 2023 na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Muwsa, Innocent Lugodisha wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya siasa ya Wilaya ya Moshi Vijijini, walipofika kuanguka maendeleo ya mradi huo ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa utekekezaji wa ilani ya chama hicho.
Amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha Mita za ujazo 2,592 kwa siku na kukamilika kwake kumeboresha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya Kata ya Njiapanda na maeneo jirani ikiwemo Miwaleni na Mabungo.
Amesema kabla ya kukamilika kwa mradi huo, upatikanani wa maji Kata ya Njiapanda ulikuwa ni mita za ujazo 770 kwa siku, huku mahitaji yakiwa ni mita za ujazo 1,190 kwa siku hivyo kukamilika kwa mradi huo, kumemaliza kabisa mgao wa maji uliokuwa ukiwakabili wananchi wa maeneo hayo.
"Kukamilika kwa mradi huu ni ukombozi kwa wananchi wa Kata ya Njiapanda, maana kwa sasa wanapata maji kwa saa 24 na kimsingi mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wamefikiwa na huduma hii muhimu," amesema.
Akizungumza Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Maleko ameipongeza Muwsa kwa kukamilisha mradi huo wa maji na kueleza kuwa kwa sasa wananchi wataweza kutumia muda mwingi kufanya shughuli za kimaendeleo tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo waliteseka kusaka huduma ya maji.