Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wananchi kuacha kufanya shughuli zozote zinazosababisha uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo, na kwamba mwananchi atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
RC Kagaigai ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Mabogini na Njia panda Wilaya ya Moshi, alipofanya ziara ya Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi (Muwsa) kutembelea na kukagua miradi miwili ya maji kwenye kata hizo.
Amesema bado kumekuwepo na uvamizi wa wananchi katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo baadhi yao wanaendesha shughuli za kilimo na kulisha mifugo, jambo ambalo limekuwa ni changamoto inayotishia kutoweka kwa vyanzo hivyo na kuwataka wananchi kuacha shughuli hizo na kushirikiana na mamlaka za maji kulinda na kutunza vyanzo hivyo.
"Maji ni rasilimali muhimu na adimu, maji ni nishati, maji ni chakula na maji ni uhai wa maendeleo kwa kila kiumbe, Maji yanaweza kuisha kama mazingira kwenye vyanzo vya maji hayajatunzwa na kuendelea kutunzwa ipasavyo, hivyo ni wajibu wetu sisi sote kama wadau na wananchi tushirikiane kutunza mazingira, ili maji yaendelee kupatikana kwa vizazi vya sasa na vijavyo"amesema Kagaigai.
Ameongeza kuwa "Vyanzo vya maji vikichafuliwa au kuharibiwa hakuna uhai, Maziwa, mito na Chemchemi tulizonazo hapa Mkoa wa Kilimanjaro, ni muhimu mno kwa shughuli za kijamii na kiuchumi na kutunza mazingira kwenye vyanzo vya maji ni kutunza uhai, kuimarisha nishati, kuongeza upatikanaji wa chakula na kuongeza uchumi kwa ujumla".
"Hivyo niwaase wananchi Kuacha ukataji wa miti ovyo pamoja na uchomaji moto wa misitu, kuacha shughuli za ujenzi wa nyumba za makazi na shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo yenye vyanzo vya maji, ndani ya mita 60 hupaswi kufanya shughuli za kibinadamu".
Aidha amesema mipango ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 iwe imefikisha maji kwa wananchi angalau asilimia 85% Tanzania nzima na kwamba mipango hiyo ya serikali itawezekana kama wananchi wote watashirikiana na serikali kulinda na kuvitunza vyanzo vya maji vilivyopo.
"Mpango mkubwa ni kwamba ifikapo mwaka 2025 ni lazima serikali iwe imefikisha maji kwa angalau asilimia 85 kwa wananchi na angalau kila mwananchi anapotembea mita 400 angalau akute maji na huo ndo mpango wa serikali awamu ya sita" alisema Mkuu wa Mkoa
Aidha Kagaigai alitumia pia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuitunza miundombinu ya maji ambayo inawekwa ili kuiwezesha kudumu na kuvinufaisha vizazi vya sasa na vijavyo
"Miundombinu mhilinde nyie ndio walinzi wa kwanza wa mali ambazo zinaletwa kwenu sisi tutakachowadai ni usalama wa miundombinu" alisema
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji katika kata ya Mabogini na Njia panda, Mkurugenzi wa Muwsa, Kija Limbe alisema mradi wa kata ya mabogini utavinufaisha vijiji vitano ambapo awamu ya kwanza utagharimu Sh1.8 bilioni na awamu ya pili utagharimu Sh1.3 bilioni.
Katika Mradi wa Njiapanda Limbe alisema utagharimu Sh2.3 bilioni mpaka kukamilika kwakwe ambapo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa maji unayoikabili kata hiyo kwa sasa.