Media Centre » Announcements

Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso Azinduzi Bodi ya nane ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA)

Mheshimiwa Jumaa Aweso amewaonya maofisa watumishi kuacha kuwa miungu watu ofisini na badala yake kutumia dhamana waliyopewa kutatua changamoto zinazowakabili watumishi ili kuwawezesha kutekeleza vyema majukumu yao.

Waziri Aweso ametoa rai hiyo wakati wa halfa ya uzinduzi wa bodi ya nane ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa)

Amesema katika baadhi ya mamlaka, maofisa utumishi badala ya kushughulikia changamoto za watumishi, wamekuwa sehemu ya kuwaumiza.

"Ni aibu, wakati mwingine tumeshuhudia, baadhi ya maofisa utumishi, wamekuwa miungu watu, wamekuwa sehemu ya kuwaumiza watumishi, kuna watu wameumizwa na kuharibiwa maisha, tambueni hii ni dhamana, leo wewe keshi atakuwepo mwingine, tusisahau tunadili na binadamu wenzetu," amesema Waziri Aweso.

Ameongeza kuwa "Siyo mtu amepata changamoto tunapigilia msumari, sikilizeni changamoto zao na muwasemee na kuwatetea watumishi wenu, siyo linatokea jambo dogo tu unaanza kumwambia kwa mujibu wa muongozo, hapana! Kuweni kimbilio lao."

Amesema ni jukumu pia la watumishi kuweka kipaombele katika kutoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na changamoto za malalamiko ya bili za maji.

Aidha Aweso ameiagiza bodi ya wakurugenzi kwa kushirikiana na menejimenti, kuweka mikakati ya kupunguza kiasi cha upotevu wa maji kutoka asilimia 27.35 ya sasa hadi kufikia chini ya asilimia 20.

"Nimesikia changamoto ya kuongezeka kwa kiasi cha maji yanayopotea kutoka asilimia 20.2 hadi kufikia asilimia 27.35, naomba tusiwe na taarifa za mazoea, hamuwezi tu kusema maji yanapotea, kwani ukweli ni kwamba zipo taasisi na hoteli makubwa wanaiba maji,  naiagiza bodi ya wakurugenzi kwa kushirikiana na menejimenti kuweka mikakati ya  kupunguza upotevu huu hadi kufikia chini ya asilimia 20," amesema.

Katika hatua nyingine, Aweso ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Muwsa kusimamia maslahi ya watumishi na kuhakikisha mwezi huu wanapandisha mishahara ya watumishi.

"Naielekeza bodi ya wakurugenzi, kushughulikia maslahi ya watumishi na mwezi huu wa tatu mishahara ya watumishi Muwsa ipande, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora."

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Kija Limbe amesema mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupata ukinzani katika baadhi ya maeneo mapya ya huduma, ambapo baadhi ya wananchi na viongizi wa vijiji hutoa ushirikiano hafifu hivyo kukwamisha mamlaka kutekeleza miradi ya uzalishaji na usambazaji maji.

Ameiomba wizara kuongeza kasi ya kutoa fedha za mradi wa maji katika Kata 12, ili uboreshaji wa miundombinu iweze kukamilika na kuondoa changamoto ya uchakavu wa miundombinu na upotevu wa maji.

"Mamlaka ina changamoto kubwa kwenye eneo la usafishaji majitaka, ambapo mabwawa yaliyopo yana uwezo wa kutibu mita za ujazo 4,500 kwa siku na kwa sasa utumiaji umefikia mita za ujazo 4,300 hivyo kuhitaji upanuzi," amesema

"Uwepo wa mahitaji ya huduma ya majitaka kwa kiwanda cha ngozi na viwanda vingine, kunaifanya mamlaka kuhitaji kufanya upanuzi huo kwa haraka hivyo mahitaji ya fedha za utatuzi ya haraka ni sh 1.6 bilioni na ili kukamilisha utatuzi wa muda mrefu zinahitajika Sh7.61 bilioni," amesema Limbe.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Muwsa, Profesa Japhari Kideghesho miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa na mamlaka hiyo ni kuongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa mita za ujazo 31,278 kwa siku mwaka 2019 hadi kufikia mita za ujazo 43, 222 kwa siku mwaka 2022.

" Ongezeko hili linahusisha utekekezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa maji yenye thamani ya sh 3.35Bilioni lakini pia mtandao wa usambazaji wa maji uliongezeka kutoka kilometa 690.06 mwaka 2019 hadi kufikia kilomita 919.6 mwaka 2022," amesema.